UDART

UDA RAPID TRANSIT PLC

UDA RAPID TRANSIT PLC

Semina ya Mafunzo ya Udereva wa Kujihami Iliyoitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Udart Waziri Kindamba Kwa Kushirikiana na Latra.

Madereva wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka UDART wamepata fulsa ya kuhudhuria mafunzo ya udereva wa kujihami yaliyoitishwa na MKURUGENZI MKUU UDART Mh. Waziri Kindamba kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA)  tarehe 26 na 27 Juni 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Teknolojia (D.I.T) uliopo jijini Dar es Salaam.

Kupitia semina hiyo, UDART ililenga kuhamasisha utamaduni wa mafunzo endelevu miongoni mwa wafanyakazi wake. Madereva walioko mstari wa mbele katika kuhudhuria semina hiyo wanatarajiwa kuwa mabalozi wa usalama barabarani na kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya kampuni.

Katika mafunzo hayo, zaidi ya madereva 300 wa UDART walipata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kujihami barabarani ili kuhakikisha usalama wao na abiria wanaowasafirisha. LATRA kama Mamlaka husika ya maswaala haya ya Usafirishaji iliona umuhimu wa mafunzo haya katika kupunguza ajali za barabarani na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yalihusisha mada mbalimbali ikiwemo: jinsi ya kuepuka ajali, umuhimu wa kutii sheria za barabarani, na jinsi ya kutambua na kushughulikia hatari zinazoweza kutokea barabarani. Vilevile, madereva walifundishwa kuhusu mbinu za kupunguza uchovu na kuongeza umakini wakati wa kuendesha magari.

Bw. Jonathan Mmali, Mkufunzi wa mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo ya udereva wa kujihamini muhimu sana kwa madereva wa magari ya usafiri wa umma kama UDART.    “Madereva wa UDART wanakutana na changamoto nyingi barabarani, hivyo ni muhimu kuwapa elimu ya jinsi ya kujihami na kujilinda ili kuhakikisha usalama wa abiria wao,” alisema Bw. Jonathan Mmali.

Madereva walioshiriki mafunzo hayo walionyesha furaha na shukrani kwa MKURUGENZI MKUU WA UDART Waziri Kindamba kwa kuruhusu kuwaandaliwa mafunzo hayo.  Bi. Naetwe H. Ihema , dereva wa UDART kwa zaidi ya miaka mitatu, alisema kuwa mafunzo hayo yamempa uelewa mpya na kumuongezea maalifa kuhusu udereva wa kujihami na pia kujua zaidi kuhusu usalama barabarani. “Nimejifunza mengi kuhusu jinsi ya kujilinda na kuwahakikishia usalama abiria wangu. Ninaamini kuwa mafunzo haya yatatusaidia sana kuboresha huduma zetu,” alisema Bi. Ihema.

LATRA iliahidi kuendelea kutoa mafunzo kama haya mara kwa mara kwa kushirikiana na UDART ili kuhakikisha kuwa madereva wote wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka  wanakuwa na ujuzi wa kutosha kwa kuongeza maarifa katika udereva wa kujihami na kuendesha kwa umakini.

Semina hiyo imekuja wakati ambapo MKURUGENZI MKUU WA UDART Waziri Kindamba anamatazamio makubwa ya kufanya maboresho ya kila nyanja ndani ya Kampuni ya Mabasi yaendayo haraka UDART, hii ikiambatana na dhamira yake ya kutaka UDART kuwa taasisi inayomjali zaidi mteja wake.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za UDART katika kuboresha viwango vya usalama na ufanisi katika huduma zake za usafiri wa umma. Kwa kushirikiana na LATRA, UDART inalenga kuhakikisha madereva wake wanakuwa na ujuzi wa kutosha katika udereva wa kijihami, hivyo kuimarisha usalama wa abiria na jamii kwa ujumla.

Kupitia semina hiyo, UDART inalenga pia kuhamasisha utamaduni wa mafunzo endelevu miongoni mwa wafanyakazi wake wote, hususani madereva walioko mstari wa mbele katika kuhudhuria semina ambapo wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani na kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya kampuni ya mabasi yaendayo haraka UDART.

Share With Friends

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

Recent Posts

Scroll to Top